Jumamosi , 9th Jul , 2016

Hafla ya kukabidhi tuzo mbalimbali za washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu wa 2015/2016 itafanyika Julai 17 mwaka huu

Nembo [logo] ya ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Jumla ya tuzo 13 za Ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania ikijulikana kama VPL zitatolewa katika hafla hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam, na kuratibiwa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kamati hiyo inaundwa na waandishi wa habari za michezo, makocha, viongozi (administrators) na wawakilishi kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo.

Tuzo hizo zitakazotolewa ni pamoja na zile za mabingwa, makamu bingwa, mshindi wa tatu, mshindi wa nne ambazo tayari zilishajulikana zinakwenda kwa timu gani nne za juu katika ligi hiyo ambayo bingwa ni Yanga akifuatiwa na Azam FC huku wekundu wa Msimbazi Simba wakishika nafasi ya tatu na wanne ni maafande wa jeshi la Magereza kutoka jijini Mbeya timu ya Tanzania Prisons.

Tuzo nyingine ambazo zitajulikana siku hiyo ya halfa ni pamoja na tuzo ya timu yenye nidhamu, mfungaji bora, mchezaji bora wa Ligi, kipa bora, kocha bora, mchezaji bora chipukizi, mchezaji bora wa kigeni, goli bora la msimu na mwamuzi bora.

Waliopendekezwa na majina yao na ya timu zao kwenye mabano (nominees) katika tuzo hizo ni kwanza wakuwania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ni wachezaji Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar), Juma Abdul (Yanga) na Mohamed Hussein (Simba) wakati kwa upande wa kipa bora ni Aishi Manula (Azam), Beno Kakolanya (Tanzania Prisons) na Deogratius Munishi (Yanga).

Kocha bora wapo Hans Van Pluijm (Yanga), Mecky Maxime (Mtibwa Sugar) na Salum Mayanga (Tanzania Prisons). Waliopendekezwa kuwania tuzo ya mchezaji bora chipukizi ni Farid Mussa (Azam), Mohamed Hussein (Simba), Mzamiru Yasin (Mtibwa Sugar) na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar).

Waliongia kwenye orodha ya tuzo ya mchezaji bora wa kigeni ni Donald Ngoma (Yanga), Thabani Kamusoko (Yanga) na Vincent Agban (Simba). Waamuzi bora katika kinyang'anyiro hicho ni Anthony Kayombo, Ngole Mwangole na Rajab Mrope.

Meneja Uhusiano wa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amewapongeza wateule wote waliopendekezwa kuwania tuzo hizo. "Kama wadhamini tuna matumaini makubwa kuwa msisimko wa ligi hii utazidi kuongezeka katika msimu ujao na kuzidi kuwapatia mashabiki wa soka wanaoifuatilia hapa nchini na nje ya nchi."

Amesema kampuni hiyo itaendelea kudhamini ligi hiyo kubwa ya soka nchini ili kutekeleza moja ya malengo yao ya kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji nchini. Pia kuwawezesha wachezaji kujipatia ajira na kuboresha maisha yao kupitia sekta ya michezo bila kusahau kuwapatia burudani wateja wake na Watanzania wote kwa ujumla.