Jumatatu , 23rd Jul , 2018

Katika michezo ya robo fainali ya Sprite Bball Kings iliyofanyika Jumamosi Julai 21, 2018 kwenye uwanja wa taifa wa ndani jumla ya wachezaji 7 waliweza kufunga pointi zaidi ya 20 kwenye mechi zao.

Moja ya michezo ya robo fainali ya Sprite Bball Kings

Orodha hiyo imeongozwa na David Godfrey, ambaye amekuwa mchezaji bora wa wiki mara mbili mfululizo akianza na ile wiki ya hatau ya 16 bora alipofunga pointi 41 kati ya 98 ilizopata timu yake dhidi ya Air Wing waliopata 78. 

Kwenye robo fainali David amefunga pointi 32 kati ya 67 ilizopata timu yake huku ikipoteza dhidi ya Mchenga Bball Stars kwa pointi 84. Katika mchezo huo David pia alipata 'Rebounds' 12 na kutoa 'Assist' 3. Lakini bahati mbaya timu yake haijasonga mbele.

Nafasi ya pili imekamatwa na Denis Babu wa Portland ambaye amefunga pointi 31 kati ya 83 ilizopata timu yake dhidi ya 70 za Temeke Heroes. Pia Babu alipiga 'Rebounds' 9 na kutoa 'Assist' 4 katika mchezo huo.

David Godfrey

Nafasi ya tatu amesimama Baraka Mopele wa Flying Dribblers ambaye alifunga pointi 25, 'Rebounds' 7 na 'Assist' 1 wakati timu yake ikishinda kwa pointi 100 dhidi ya 67 za Water Institute. Felix Deogratus wa Water Institute ameshika nafasi ya tatu baada ya kupata pointi 25, 'Rebounds' 5 na 'Assist' 1 timu yake ikipoteza dhidi ya Flying Dribblers.

Maselo Nyirabu wa Mchenga Bball Stars ameshika nafasi ya tano akifunga pointi 24, Rebounds 6 na Assist 2 timu yake ikishinda kwa pointi 83 dhidi ya 67 za St. Joseph. Yasin Fundi yeye amechukua nafasi ya 6 akifunga pointi 23, Rebounds 6 na Assist 2. Abdul Chimgwengwe amefunga 22, 'Rebounds' 3 na 'Assist' 2 akishika nafasi ya 7.