Jumanne , 22nd Dec , 2020

Ligi kuu soka Tanzania bara raundi ya 17, itaanza kutimua vumbi hii leo kwa michezo 4, ikiwa ni michezo yakukamilisha michezo ya duru la kwanza, michezo ya leo itachezwa Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara.

Michezo 4 raundi ya 17 VPL, kuchezwa leo katika viwanja 4 tofauti

Mchezo wa mapema leo utachezwa Saa 8:00 mchana, katika dimba la Gwambina Complex, Gwambina FC watakuwa wenyeji wa Mbeya City, Gwambina wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa juu ya Mbeya City kwa tofauti ya alama 6, Gwambina wana alama 18 wakiwa nafasi ya 12 wakati Mbeya City wapo nafasi ya 17 wakiwa na alama 12.

Mchezo huu utakuwa wa kwanza kwa timu hizi kukutana katika michezo ya ligi kuu.

Saa 10:00 jioni itachezwa michezo 3, katika dimba la Mwadui Complex, Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Coastal Union ya Tanga, msimu uliopita kwenye dimba la nyumbani, Mwadui FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal.

Wenyeji Mwadui wanashuka dimbani wakiwa wanaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na alama 11 na hawajashinda mchezo hata mmoja katika michezo yao 9 ya mwisho, wakati Coastal wapo nafasi ya 13 wakiwa na alama 18.

Uwanja wa Karume Mara, Biashara United watakipiga dhidi ya Tanzania Prisons, timu hizi zinatofautiana alama 2 kwenye msimamo, Biashara wapo juu ya Prisons wakiwa na alama 23 wakiwa nafasi ya 5 wakati Prisons wana alama 21 wakiwa nafasi ya 9.

Katika michezo 4 ya ligi ambayo timu hizi zimekutana limefungwa bao 1 tu, ilikuwa msimu uliopita ambapo Biashara United iliibuka na ushidni wa bao 1-0, katika dimba la Karume, lakini michezo mingine 3 yote ilimalizika kwa suluhu.

Mchezo mwingine utachezwa mkoani Kagera, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Polisi Tanzania ya Moshi.

Msimu uliopita Polisi walishinda michezo yote miwili mbele ya Kagera, ukiwemo ushindi wa mabao 2-1, kwenye uwanja wa nyumbani wa Kagera dimba la Kaitaba, timu hizi zinaingia kwenye mchezo wa jioni ya leo zikiwa na tofauti ya alama 1 tu. Polisi Tanzania wapo nafasi ya 6 wakiwa na alama 22, wakati Kagera wana alama 21 wakiwa nafasi ya 10.