Alhamisi , 3rd Oct , 2019

Ikiwa imebakia siku moja pekee kabla ya vumbi kutimka katika Uwanja wa Don Bosco Oysterbay katika fainali ya Sprite Bball Kings 2019, baadhi ya mastaa wa timu zilizofuzu fainli wameelezea safari za maisha yao ya mpira wa kikapu.

Baadhi ya wachezaji wa Tamaduni na Mchenga Bball Stars

Fainali hiyo inatarajia kupigwa kesho Ijumaa, Oktoba 4 kuanzia saa 10:00 jioni ambapo mabingwa watetezi na wa kihistoria wa mashindano hayo, Mchenga Bball Stars itakapopambana na Tamaduni.

Mchezaji wa kwanza aliyezungumza ni Baraka Mopele wa Tamaduni ambaye amesema kuwa ni mchezaji wa Vijana City Bulls, pia amewahi kucheza ligi ya kikapu ya Uganda. Uzoefu alionao ni kucheza michuano ya 'East and Central Africa Zone 5'  na kwamba amejipanga kucheza fainali ya mwaka huu akitarajia kuchukua ubingwa.

Baraka Sadick wa Mchenga Bball Stars yeye anachezea timu ya JKT, amewahi kuwa MVP wa Sprite Bball Kings 2018, amewahi kucheza timu ya taifa ya kikapu, alishiriki kwenye michuano ya 'Qualifier Zone 5' na amejipanga na timu yake ya Mchenga kushinda ubingwa wa Sprite Bball Kings 2019.

Ashraf Haroun wa Tamaduni yeye ni mchezaji na kocha wa timu ya Vijana, mmoja ya makocha wa timu ya taifa ya kikapu ya Tanzania akiwa na timu ya Tamaduni kwa msimu wa tatu mfululizo.

Mwingine aliyezungumza ni Isaya Swile wa Mchenga Bball Stars ambaye ni kwa mara ya kwanza anashiriki michuano hii, akisema kuwa amejiunga nao akijua kuwa ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo na lengo lao kuu ni kuhakikisha Mchenga inabeba tena ubingwa.