Alhamisi , 3rd Dec , 2020

Cristiano Ronaldo amewashukuru makocha, wachezaji na timu pinzani baada ya kufikisha idadi ya mabao 750. Ronaldo alifunga bao 1 kwenye ushindi wa mabao 3-0 walioupata Juventus kwenye mchezo wa Ligi ya Mabaingwa Ulaya dhidi ya Dynamo Kiev.

Cristiano Ronaldo amefunga mabao mengi zaidi akiwa na klabu ya Real Madrid, amefunga mabao 450 katika michezo 438

Ronaldo ambaye ni mchezaji bora wa Dunia mara 5, alifunga bao lake la 75 tangu ajilunge na Juventus na la 750 dakika ya 57 ya mchezo dhidi ya Dynamo Kyiv katika mchezo wa kundi G.

Baada ya kufikia idadi hiyo ya mabao Ronaldo aliandika katika ukarasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

"Magoli 750, nyakati 750 za kufurahisha, tabasamu 750 katika nyuso za mashabiki wetu. Asante kwa wachezaji na makocha wote ambao walinisaidia kufikia idadi hii ya kushangaza, asante kwa wapinzani wote ambao walinifanya nifanye nijitume kila siku."

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 35, amefunga mabao mengi zaidi akiwa na klabu ya Real Madrid, ambapo alifunga mabao 450 katika michezo 438, katika miaka yake 6 akiwa na kikosi cha Manchester United alifunga mabao 118, lakini pia alifunga mabao 5 katika michezo 31 akiwa na kikosi cha Sporting CP, amabyo ni timu ya nyumbani kwao Ureno.

Ronaldo, ambaye hivi karibuni alifikisha mabao 102 kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ureno, na kuwa mwanasoka wa pili wa kiume kufikia idadi ya mabao 100 kwenye timu za taifa, nyuma ya Ali Daei wa Iran.

Makocha waliowahi kumfundisha Ronaldo ni Alex Ferguson, Jose Mourinho, Carlo Ancelotti na Zinedine Zidane. Pia mshambuliaji huyo ameshinda jumla ya mataji 30 ukiwemo ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya mara 5, na ubingwa wa ulaya kwa timu za taifa EURO mara 1.