Jumanne , 26th Oct , 2021

Kocha wa magolikipa wa Taifa Stars, Ivo Mapunda amesema kuwa kuna mabadiliko makubwa kwenye upande wa idara ya walinda mlango, ambapo asimilia 75% sasa ni kuchezea mpira mguuni kuliko kudaka kama ilivyokuwa miaka ya zamani.

Aishi Manula(Kushoto) na Djigui Diarra (Kulia).

Mapunda amesema hayo huku akimwagia sifa mlinda mlango wa Yanga, Djigui Diarra, kuwa anajicho kubwa la kuusoma mchezo na msaada mkubwa hasa kwenye kuanzisha mashambulizi pamoja na utulivu awapo uwanjani.

Katika kuthibitisha kauli ya Mapunda, Golikipa huyo raia wa Mali alipiga mpira mrefu uliozaa bao la Fiston Mayele katika mechi ya Yanga dhidi ya Simba na kusaidia timu yake kutwaa ubingwa Ngao ya jamii.

Vilevile Mapunda amemwagia sifa golikipa wa Simba, Aishi Manula kuwa na uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi akitolea mfano kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji alisaaidia timu yake kushinda mchezo huo baaada ya kupiga mpira mrefu uliotua kwa Chris Mugalu aliyeudondosha kwa mfungaji wa bao meddie Kagera.

Vilevile mchezaji huyo wa zamani Simba na Yanga, amesema kuwa ni wakati wa Shirikisho la soka nchini (TFF) kuipa thamani nafasi ya makocha wa magolikipa kwa kuanzisha tuzo zao.

Idara hiyo imekuwa inajitegemea kwasababu magolikipa wapo chini ya usimamizi wa makocha wao binafsi tofauti na wale wanaocheza nafasi za ndani ya kiwanja.