Jumamosi , 12th Mar , 2016

Baada ya kupita bila jasho katika mzunguko wa awali kufuatia timu ya Gaborone United kujitoa na hatimaye kutinga mzunguko wa kwanza timu ya JKU yaanza kutoka jasho baada ya kukumbana na kibano kizito toka kwa vijogoo wa Kampala Sports Club Villa.

Kikosi cha timu ya JKU ya Zanzibar ambacho leo hii kimepoteza mchezo wao dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda.

Kikosi cha maafande wa Jeshi la Kujenga Uchumi visiwani Zanzibar timu ya JKU hii leo ikiwa ugenini katika uwanja wa Nakivubo jijini Kampala nchini Uganda imeanza vibaya mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kukubali kichapo kizito cha mabao 4-0 toka kwa wenyeji wao vijogoo wa jiji la Kampala timu ya Sports Club Villa.

Pamoja na JKU kuonekana kana kwamba pengine isingefungwa idadi hiyo kubwa ya magoli hasa kwa jinsi ilivyouanza kwa kasi mchezo huo katika dakika tano za mwanzo lakini mambo yakageuka mapema kunako dakika ya tisa tu ya mchezo pale vijogoo wa Kampala walipoanza kuhesabu karamu ya magoli kupitia kwa goli safi la mshabmuliaji Ndera Mike.

Mchezo uliendelea huku kila timu ikiishambulia nyingine kwa zamu lakini ilikuwa ni Villa tena kunako dakika ya 34 ikafanikiwa kuandika bao la pili kupitia kwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Serugamba Mike na hadi timu zinakwenda mapumziko Villa ilikuwa mbele kwa bao hizo mbili.

Kipindi cha pili kunako dakika ya 47 dakika mbili tangu kuanza kipindi hicho wenyeji Sports Club Villa wakaandika bao la tatu kupitia kwa mchezaji Kasumba Umar na karamu ya mwisho ya mabao ya timu hiyo ilihitimishwa kunako dakika ya 62 kwa bao safi la shuti kali la kiufundi lililokwamishwa wavuni na mshambuliaji Lwesibawa Godfrey na hadi mwisho wa mchezo Villa imeibuka na ushindi huo mnono wa bao 4-0 nakujiweka katika mazingira mazuri ya kuvuka hatua hiyo.

Na kwa matokeo hayo ya kipigo hicho kikubwa kwa wawakilishi pekee wa Zanzibar katika michuano ya kimataifa timu ya JKU baada ya mafunzo kuondolewa na Vita Club ya DR Congo katika hatua ya awali ya ligi ya mabingwa sasa maafande hao ambao walitinga hatua hiyo baada ya timu ya Gaborone United ya Botswana kujitoa sasa JKU watalazimika kupanda mlima mrefu ili kushinda mchezo wa nyumbani si kwa chini ya mabao 5-0 ili ivuke kizuizi hicho wiki mbili zijazo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa katika uwanja wa Aman visiwani Zanzibar.