Mashabiki wa Simba SC
Mchezo huu unachezwa Saa 10:00 Jioni uwanja wa Benjamini Mkapa Jiji Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa kundi D.
Kuelekea mchezo huu Nahodha wa kikosi cha Simba SC John Bocco amesema wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa hawana presha kwa kuwa wapo nyumbani na wamejipanga kushinda.
“Tunaiheshimu ASEC ni timu bora na ina wachezaji wazuri lakini hatuigopi wala hatutaingia kwa presha. Tumejiandaa vizuri kimwili na kiakili kuhakikisha tunaibuka na ushindi. Kikubwa nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kuja kutupa sapoti, tunaamini tutawapa furaha kwa kupata ushindi,” amesema Bocco.
Kikosi hicho cha mabingwa wa Tanzania bara kitawakosa nyota wake kadhaa kutokana na majeruhi akiwemo Shomari Kapombe, Kibu Denis, Hassan Dilunga, Taddeo Lwanga na Clatous Chama ambaye anakoseka kwa sababu za kikanuni kwa sababu msimu huu alishacheza kwenye michuano hii akiwa na kikosi cha RS Berkane kabla ya kujiunga na Simba kipindi cha dirisha dogo la usajili.
ASEC wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja kwenye michezo 9 ya mwisho kwenye michuano yote, lakini mara ya mwisho kucheza mchezo wa kimashindano ilikuwa Disemba 29, 2021 baada ya Ligi ya Ivory Coast kusimama kupisha michuano ya AFCON.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa mwaka 2003 kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika hatua ya makundi na timu hizi zilikuwa kundi A, mchezo wa kwanza Simba walishinda Dar es salaam bao 1-0 na mchezo wa marejeano Asec waliifunga Simba mabao 4-3 Ivory Coast.
Mmchezo mwingine wa kundi hili utachezwa Saa 4:00 Usiku ambapo klabu ya RS Berkane ya Morocco watakuwa weneji wa US Gendamerie ya Niger.

