Jumatatu , 2nd Mei , 2016

Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),leo saa 5:00 asubuhi itatangaza uamuzi wa rufaa nane zilizowasilishwa na kujadiliwa za viongozi, mchezaji na timu tatu zilizoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania

Jengo la ofisi za makao makuu ya shirikisho la soka nchini Tanzania TFF zilizoko maeneo ya Karume jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo itatangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa ofisi za TFF, zilizoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Jumla ya rufaa nane zinazohusu timu, kocha, viongozi na mchezaji mmoja zilijadilikuwa na kamati hiyo kwa Jumapili Mei mosi, 2016 kwenye ofisi za TFF jijini.

Rufaa zilizojadiliwa kwenye kikao hicho ni za:

1. Timu ya Geita Gold

2. Choki Abeid ambaye ni Kocha Msaidizi wa timu ya soka ya Geita Gold FC

3. Denis Richard Dioniz - Kipa wa Geita Gold

4. Fatel Rhemtullah – Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora

5. Saleh Mang’ola – Mwamuzi wa Soka wa Mkoa wa Dodoma

6. Timu ya Soka ya Polisi Tabora

7. JKT Oljoro Fc ya Arusha

8. Yusufu Kitumbo – Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora

Wadau hao wa soka walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu baada ya kamati hiyo kuwatia hatiani na kuwaadhibu kwa makosa ya kupanga matokeo ya michuano ya Ligi Daraja la Kwanza. Wakata rufaa wote walihudhuria kikao cha rufaa zao.

Wakati huo huo Kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kinafanyika kesho Jumanne Mei 3, 2016 kwenye ukumbi wa ofisi za shirikisho zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho cha kupitia mashauri mbalimbali yaliyowasilishwa TFF, ilikuwa kifanyike Jumapili Mei Mosi, lakini kiliahirishwa kwa sababu ya wajumbe wengi walikuwa na udhuru.

Wadau watakaojadiliwa kesho ni pamoja na Kocha Mkuu wa Azam FC ya Dar es Salaam, Stewart Hall na wachezaji wake wakiwamo John Bocco, Shomari Kapombe, Aishi Manula na Kipre Tchetche.

Wengine ni nyota wa Young Africans SC ya Dar es Salaam ambao ni Amissi Tambwe na Donald Ngoma wakati kutoka timu ya JKT Rwakoma ya Mara wamo Paulo Jinga, Zephlyn Laurian na Idrisa Mohamed.

Wengine ni Ismail Nkulo, Said Juma, Idd Selaman na Edward Amos wa Polisi Dodoma, kadhalika Abel Katunda wa Transit Camp ya Dar es Salaam na daktari wa Coastal Union ya Tanga, Dk. Mganaga Kitambi.

Pia Herry ‘Mzozo’ Chibakasa wa Friends Rangers ya Dar es Salaam naye atajadiliwa na Bunu Abdallah ambaye ni Kocha Msaidizi wa JKT Oljoro ya Arusha.