Jumanne , 6th Dec , 2022

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha ametoa wito kwa waogeleaji kwenda kupambana kufa na kupona Ili kufanye vizuri katika mashindano ya Dunia ambayo yanatarajia kuanza Disemba 13 hadi 19 mwaka huu nchini Australia.

Msitha ameyasema hayo leo Disemba 06, 2022 wakati akiwaaga na kuwakabidhi bendera waogeleaji wa timu ya Taifa watakaoiwakilisha nchi katika michuano hiyo ambao wanatarajia kuondoka Disemba 08 nchini kuelekea katika mashindano hayo.

Amewataka wachezaji hao kwenda kuitangaza Tanzania kupitia utamaduni wake, lugha ya kiswahili  na kuipeperusha bendera ya Taifa vyema pamoja na kuzingatia nidhamu.

"Leo tunawakabidhi bendera hii  na mnabeba jukumu la watanzania  kwa kuitangaza nchi na mkaipeperushe vyema bendera na sina mashaka na maandalizi yenu nawaamini, msiende kinyonge serikali tupo pamoja nanyi," amesema.

Msitha ameyaomba makampuni kujitokeza kuwekeza katika michezo mingine ukiwamo wa kuogelea Ili kutoa fursa sambamba na vyama vya michezo kuiga programu za kuibua vipaji ambavyo vitasaidia kuchagua wachezaji  bila upendeleo.

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) Asma Hilal, àmesema wachezaji wapo tayari kwenda kupambana  ili warudi na matokeo mazuri na ahadi kwa watanzania watafanya vizuri, huku akiwaomba watanzania kuwaombea dua na maombi timu iweze kufanya vizuri na kupeperusha bendera ya Taifa vyema.

Kwa upande wa Kocha wa timu hiyo Alex Mwaipasi ametaja wachezaji wanne watakaoiwakilisha nchi kuwa ni pamoja na Collin Saliboko, Hilal Hilal, Ria Save na Sophia Latiff.

Aliongeza kuwa wataendelea kutunza heshima na hayo mashindano ni kipimo chao cha Daraja la Kimataifa ikiwa kiu yao ni kufuzu kimataifa na walichofanya katika mashindano yaliyopita wataongeza .

Kwa niaba ya wachezaji Collins Saliboko, alisema wamejipanga vizuri  na lengo lao kuu ni kuhakikisha wanapunguza muda na kufikia olimpiki.