Jumanne , 18th Dec , 2018

Baada ya hapo jana kocha wa Yanga Mwinyi Zahera kuondoka nchini kuelekea Ufaransa, maelezo ya safari yake yamegubikwa na utata mtupu baada ya viongozi pamoja na yeye mwenyewe Zahera kutofautiana katika maelezo yao.

Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika na kocha Mwinyi Zahera

Kwa mujibu wa Mwinyi Zahera, yeye amesema ameenda kusaini nyaraka zinazohusiana na biashara zake hivyo atakaa hadi Desemba 25 na atarudi Dar es salaam Desemba 26 asubuhi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, yeye amesema Kocha Mwinyi Zahera amekwenda Ufaransa kwa ajili ya kushughulikia kesi ya mkewe ambayo hakufafanua inahusu nini.

Mapema jana Desemba 17, 2018 asubuhi, msemaji wa Yanga, Dismas Ten, alisema Kocha Zahera ameenda Ufaransa kwa ajili ya matibabu ambayo yanaratibiwa na chama cha soka nchini DR Congo.

Kabla ya safari yake kocha Mwinyi Zahera alieleza kuangushwa kwake na viongozi wa Yanga hususani kamati ya usajili baada ya kushindwa kukamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji ambao alipendekeza waongezwe kikosini.