Alhamisi , 18th Dec , 2014

TIMU ya Vijana ya Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kutinga hatua ya Nusu Fainali baada ya kuishinda timu kutoka mkoa wa Mwanza katika michuano ya Copa Coca Cola ngazi ya Taifa iliyochezwa leo uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Kocha wa Timu ya Mkoa wa Kigoma, Hamis Mabo amesema vijana wake walitumia sehemu ya makosa ya wapinzani wao hivyo kufanikiwa kuibuka na ushindi wa Goli 1-0.

Mabo amesema hatua waliyoifikia katika michuano hiyo ni nzuri hivyo wanategemea kuendelea kufanya vizuri zaidi na hatimaye kuibuka na ushindi.

Kwa upande wake kocha kutoka Timu ya mkoa wa Mwanza, Ahamed Simba amesema kushinda na kushindwa ni sehemu ya mchezo, hivyo kwa hatua waliyoifikia sio mbaya sana kwani ameweza kutambua makosa yaliyopo katika timu yake hivyo anayo nafasi kubwa ya kuweza kuyarekebisha.

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Parkers jijini Dar es salaam, Timu ya vijana kutoka mkoa wa Morogoro imeondolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa na timu ya vijana kutoka mkoa wa Dodoma baada ya kufugwa goli 2-1 na kupelekea timu kutoka mkoa wa Dodoma kutinga hatua ya Nusu Fainali katika michuano hiyo.