Jumamosi , 9th Dec , 2017

Timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imetupwa nje ya michuano ya CECAFA Senior Challenge inayoendelea nchini Kenya baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Rwanda mchana huu.

Baada ya kupoteza mchezo wa leo Kilimanjaro inakuwa imefungwa michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja hivyo kubakiza mchezo mmoja ambao hata ikishinda itafikisha alama 4 ambazo haziwezi kuisadia kuendelea na hatua inayofuata,

Rwanda wamefungua ukurasa wa mabao mapema dakika ya 17 kupitia kwa Innocent Nshuti  lakini Kilimanjaro walifanikiwa kusawazisha dakika ya 29 kupitia kwa mshambuliaji Danny Lyanga.

Bao la ushindi la Rwanda ambalo limewatoa mashindanoni Kilimanjaro Stars limefungwa kipindi cha pili dakika ya 66 kupitia kwa Biramahire Abeddy.

Kilimanjaro ilitoka sare na Libya kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Zanzibar Heroes siku ya Alhamisi. Kilimanjaro sasa imebakiwa na mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba katika kundi A dhidi ya wenyeji Kenya.