Kocha Matola awasumbua wazungu Simba, Azam FC

Jumatatu , 11th Feb , 2019

Kocha Mkuu wa klabu ya Lipuli FC, Seleman Matola anayo rekodi nzuri msimu huu dhidi ya makocha wa kizungu wanaofundisha Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na Azam FC.

Lipuli FC dhidi ya Simba na Azam FC

Lipuli FC imecheza mechi mbili kubwa ugenini dhidi ya makocha, Patrick Aussems wa Simba katika uwanja wa taifa na Hans Van der Pluijm wa Azam FC katika uwanja wa Chamazi na kupata sare.

Matola amesema kuwa kikosi chake hakina hela ila atapambana kuwamaliza matajiri wa Dar es Salaam, Azam FC katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa hii leo mjini Iringa.

"Hatukutegemea kuwa katika hali kama hii kwenye Ligi Kuu Bara hasa baada ya kuwakosa wadhamini, timu inapitia katika mazingira magumu ila wachezaji wamekubaliana na hali wanapata matokeo uwanjani", amesema Matola.

Pia amesema benchi lake la ufundi lilikaa na wachezaji na kuwajenga kisaikolojia. Sasa akili zao zimeelewa ni mwendo gani wanatakiwa kwenda nao.

"Tutakutana na wapinzani wetu ambao wapo vizuri kiuchumi ila nina imani tutabakiza pointi zetu hapa", ameongeza Matola.

Lipuli FC ipo nafasi nne za juu za ligi, ikiwa na pointi 36 mpaka sasa baada ya kushuka dimbani katika michezo 24, huku Azam FC ikiwa na pointi 48 baada ya kushuka dimbani michezo 21.