Ijumaa , 10th Jul , 2020

Uongozi wa klabu ya Lipuli ya mkoani wametakiwa kutatua mgogoro uliopo baina yao na wachezaji ili kuinusuru timu hiyo kuporomoka daraja.

Mshambuliaji kinara wa mabao wa Lipuli Paul Nonga(Pichani) akishangilia katika moja ya bao aliloifungia timu yake,lakini nyota huyo hayupo kikosini akishinikiza malipo yake.

Kauli hiyo imetolewa na kocha mkuu wa kikosi hicho, Nzayimana Mailo ambaye amesema anasikitishwa na namna wachezaji wake wanavyogombana uwanjani na hata kushindwa kutekeleza maagizo yake kiasi cha kufungwa michezo muhimu.

Nzayimana ambaye jana alishuhudia kikosi chake kikifungwa na Alliance mabao 2-0 katika uwanja wa Nyamagana,amesema wachezaji wake walijua wanahitaji ushindi lakini walijawa na mashaka ambayo anaamini kuna kitu kinaendelea ndani ya nafsi zao.

Katika hatua nyingine, kocha huyo raia wa Burundi ameongeza kuwa timu yake inapoteza nafasi ya kufunga mabao kutokana na kuwa wachezaji wengi wa Tanzania wamejifunza mpira ukubwani jambo ambalo linawapa wakati mgumu makocha.

Ikumbukwe Lipuli imetajwa kuwa na mgogoro na wachezaji wake walioripotiwa kudai mishahara yao,huku baadhi yao akiwemo aliyekua nahodha na mshambuliaji kinara Paul Nonga kugoma kurejea kikosini.

Wanapaluhengo walikua bora katika misimu yao miwili ya mwanzo tangu wapande ligi kuu, lakini hivi sasa wanashika nafasi ya 17 wakia na alama 37 na iwapo watashindwa kuzichanga karata zao vyema huenda wakawa miongoni mwa timu 4 zitakazoshuka daraja msimu huu moja kwa moja.