Alhamisi , 28th Jan , 2021

Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel amesema malengo ya kikosi chake msimu huu ni kuhakikisha wanamaliza kwenye nafasi 4 za juu kwenye msimamo wa ligi kuu England na sio kuwania ubingwa hii ni baada ya kikosi hicho kutoka suluhu na Wolves kwenye mchezo wa EPL.

Chelsea imeshinda michezo 2 tu kwenye michezo 9 ya mwisho ya EPL

Tuchel alitangazwa kuwa kocha mpya wa Chelsea siku moja iliyopita akichukua mikoba ya kocha Frank Lampard, na hapo jana akakiongoza kikosi hicho kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Wolves na mchezo huo ulimalizika kwa suluhu katika dimba la Stanford Bridge.

Baada ya mchezo huo kumalizika kocha huyo mjerumani alisema ni ngumu sana kufikiria kuhusu ubingwa.

''Ubingwa ooh, hiyo mbali sana tunapaswa kuwa wa kweli. Unapojiunga na Chelsea kama meneja ipo wazi kabisa unasaini kwa matarajio ya kushinda mataji, Ligi kuu, ligi ya mabingwa na vikombe ipo wazi kabisa. Lakini wakati huohuo lazima tuwe wakweli kuna timu nyingi na alama nyingi kati yetu na timu iliyopo nafasi ya 4''

Kwa sasa the blues wapo nafasi ya 8 kwenye msimamo wa EPL ikiwa na alama 30, wakiwa wamezidiwa alama 11 na vinara wa ligi Manchester City wenye alama 41, lakini pia wanazidiwa alama 5 na West Ham United waliopo nafasi ya 4, nafasi ambayo inatoa uwakilishi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa.

Chelsea wameshinda michezo 2 tu kwenye mechi 9 ya mwisho ya ligi kuu, huku sare ya jana ikiwa ni ya 2 kwenye michezo hiyo na wamefungwa michezo 5. Mchezo unaofata watakipiga dhidi ya Burnley katika dimba la Stanford Bridge.