Jumapili , 9th Aug , 2020

Mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski amefikisha mabao 13 kwenye michuano ya klabu bingwa ulaya baada ya kuifungia timu yake mabao mawili kwenye ushindi wa 4-1 dhidi ya Chelsea usiku wa jana. 

Mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski

Lewandowski amebakiza mabao 4 kufikia rekodi iliyowekwa na Cristiano Ronaldo ya kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja kwenye historia ya michuano hii ambayo aliiweka msimu wa 2013-14 kwa kufunga mabao 17. Lakini pia mabao hayo mawili dhidi ya Chelsea yamemfanya Lewandowski asogee mpaka nafasi ya 4 kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa michuano hii kwa kufikisha mabao 66.

Bado Lewandowski ana nafasi ya kufunga zaidi kwani kikosi cha Bayern Munich kimetinga hatua ya Robo Fainali baada ya kuiondoa Chelsea kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1 na wataminyana na FC Barcelona katika hatua ya Robo Fainali. 

Endapo Bayern watafanikiwa kutinga hatua ya fainali basi mshambuliaji huyo wakimataifa wa Poland atacheza  michezo mitatu zaidi na atajiongezea nafasi ya kufikia au kuvunja kabisa rekodi ya CR7.

Msimu huu wa 2019-20 umekuwa bora sana kwa Lewandowski mpaka sasa kafunga jumla ya mabao 53 katika michezo 44 kwenye michuano yote na akiwa amefunga mabao hayo kwenye michezo 36 kati ya 44 aliyocheza. Pia ndio kinara wa ufungaji msimu huu kwenye michuano hiyo ya ulaya na bao zake 13.