Ijumaa , 15th Jan , 2016

Baada ya kusimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara mzunguko wa kumi na nne (14) unatarajiwa kuendelea hapo kesho wikiendi hii kwa michezo 8 kuchezwa katika viwanja mbalimbali.

Uwanja wa Tafa jijini Dar es salaam, Simba SC watawakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar saa 10 jioni huku Azam FC dhidi ya African Sports ukianza saa 1 usiku na Mbeya City watakua wenyeji wa Mwadui FC uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mkwakwani jijini Tanga Coastal Union watawakaribisha Majimaji, Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, maafande wa JKT Ruvu watawakaribisha maafande wa Mgambo Shooting, Toto Africans watawakaribisha Tanzania Prisosns uwanja wa CCM Kirumba, huku Stand United wakicheza dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa mchezo mmoja uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, ambapo Young African watawakaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara.