Jumatano , 15th Jul , 2020

Gwiji wa zamani wa soka Gary Lineker amesema kuwa mara zote anafikiria kuwa mshambuliaji wa Chelsea, Olivier Giroud hapewi heshima yake anayostahili kutokana na mchango wake katika timu.

Mshambuliaji wa Chelsea Olivier Giroud (katika picha) akishangilia bao alilofunga jumanne dhidi ya Norwich City.

Lineker ambaye aliwahi kuvichezea vilabu vya Barcelona,Tottenham Hotspurs,  Leicester City, na Everton, amemuelezea Giroud kama mshambuliaji bora katika eneo la hatari pamoja na mikimbio mizuri huku akitunza mpira na kumalizia kazi ya kufunga katika nafasi muhimu.

Ameongeza kuwa inawezeka Giroud hana kasi ya kubwa lakini licha ya kasoro hiyo haimaanishi si mshambuliaji wa kiwango cha juu na anahitaji kuheshimiwa katika hilo.

Giroud amefunga katika mechi tatu za EPL alizoanza ambapo jana aliisaidia Chelsea kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Norwich City na kuwafanya The Blues kujiweka katika mazingira bora ya kumaliza kwenye nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi utakaowawezesha kushiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.

Takwimu za mshambuliaji huyo wa Ufaransa, zinaonyesha kacheza michezo 16 na kufunga mabao 6 huku katika michuano yote akifunga mabao 7 kwenye michezo 20.

Tangu mshindi huyo wa kombe la Dunia ajiunge na Chelsea mwaka juzi akitokea Arsenal, amecheza michezo 83 na ameifungia mabao 25 katika mashindno yote.