Jumatatu , 5th Jul , 2021

Arsenal na Liverpool zipo kwenye vita ya kumuwania kiungo wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Lile ya Ufaransa Renato Sanches, ambapo timu zote hizo zimeonyesha nia ya kumuhitaji na klabu yake ya Lile ipo tayari kumuuza katika kipindi hiki cha usajili.

Renato Sanches

Liverpool ndio inapigiwa chepuo kuinasa huduma ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye alitoa mchango mkubwa kwenye mafanikio ya klabu ya Lile ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa Ligue 1 kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2010-11. Ambapo alicheza jumla ya michezo 29 na kufunga bao 1.

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp anamtazama Sanches kama mbadala wa kiungo Georginio Wijnaldum aliyetimkia PSG baada ya mkata wake kuisha. Ripoti kutoka nchini Ufaransa zinaripoti kuwa Liverpool wanakutana na upinzani kutoka kwa klabu ya Arsenal ambao nao wameanza mipango ya kuhakikisha wanaisa huduma ya Sanches.

Majogoo hao wa jiji la Liverpool wanatajwa kuwawania wachezaji wengine ambao wanawaangazia kama mbadala ni kiungo wa Borussia Monchengladbach Florian Neuhaus na Yves Bissouma wa Brighton.

Kiungo huyu ni kama kazaliwa upya baada ya kupitia kipindi kigumu cha kuishi nje ya matarajio baada ya kusajiliwa na Bayern Munich msimu wa 2016-17 akitokea Benifica akiwa na umri mdogo ambapo alionyesha kiwango bora akiwa na Benifica na kufanikiwa kushinda tuzo ya mchezo boora kijana barani ulaya (Golden Boy) mwaka 2017 baada ya kujiunga na Bayern Munich akiwashinda wachezaji Marcus Rashford, Kingsley Coman na Ousmane Dembele.