Jumatatu , 7th Dec , 2020

Kocha mpya wa Azam George Lwandamina 'Chicken Man' anatazamiwa kuiongoza klabu hiyo kwa mara ya kwanza kucheza dhidi ya Gwambina kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara unaotaraji kupigwa saa 10 kamili jioni ya leo kwenye dimba la Gwambina lililopo Misungwi jijini Mwanza.

Mtendaji mkuu wa Azam Fc, Abdulkarim Amim (Kushoto),Afisa Habari Zacharia Thabit( Kulia) walipokuwa wakimpokea kocha wao mpya George Lwandamina (Katikati) ambaye leo anaanza rasmi kibarua dhidi ta Gwambina.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha msaidizi wa Azam, Bahati Vivier amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilikana na wapo tayari kuwavaa Gwambina na kuondoka na alama tatu licha ya kuthibitisha kuwakosa baadhi ya wachezaji nyota wa kikosi cha kwanza wenye majeraha.

Wachezaji ambao wamethibitishwa kukosekana ni Mlinzi wa Kati Yakubu Mohamed ambaye amepasuka juu jicho, Salum Aboubakar mwenye maumivu ya mguu aliyoyapata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Biashara Utd na Kiungo Never Tegere aliyepata maumivu ya mguu akiwa mazoezi.

Kocha msaidizi, Bahati Vivier ameendelea kwa kusema“Sisi kama benchi la ufundi la timu tumeona mapungufu na tumetumia muda wote tuliokaa Mwanza kuyafanyia kazi na wachezaji wameelewa kile ambacho tumewaambia” Vivier akizungumzia kuhusu mapungufu katika safu yao ya Ulinzi.

Kwa upande wa timu mwenyeji klabu ya Gwambina imeendelea kuwahamisha mashabiki kujitokeza uwanjani kwa wingi kushuhudia mtanange huo huku wakisisitiza kwenye kwa kuandika “Hii si yakukosa” kwenye kurasa za akaunti za mitandao yao yakijamii.

Licha ya kukosa ushindi kwenye michezo mitatu mfululizo, hivi sasa Azam bado amesalia nafasi ya pili akiwa na alama 26 tofauti ya alama 8 na kinara Yanga ilhali klabu ya Gwambina ya jijini Mwanza ipo nafasi ya 11 wakiwa wamejizolea alama 16 chini ya kocha Fulgence Novatus.