Jumapili , 5th Jul , 2020

Nyota wa klabu ya Juventus ya Italia na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, akiwa na miaka 35 ameendelea kuweka rekodi katika soka baada ya kufanikiwa kufikisha magoli 25 katika msimu mmoja wa Serie A.

Cristiano Ronaldo akipiga Freekick dhidi ya Torino

Goli la Ronaldo jana dhidi ya Torino limemfanya kuwa mchezaji wa pili kufikisha idadi hiyo ya magoli ndani ya Juventus kwa msimu mmoja tangu alipofanya hivyo mchezaji Omar Sívori msimu wa 1960/61.

Hata hivyo goli hilo alifunga kwa mpira wa adhabu ndogo au pigo huru, ambapo sasa amefunga goli lake la kwanza la Freekick tangu ajiunga na Juventus. Goli hilo limekuja katika majaribio 43 ambayo alifanya bila mafanikio.

Kwa upande mwingine golikipa mkongwe wa Juventus Gianluigi Buffon ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi 648 za Serie A.

Cristiano Ronaldo katika mechi 16 mfululizo za Serie A msimu huu ameweza kufunga goli au kutoa pasi ya goli. Katika mechi hizo 16 za mwisho amefunga magoli 20 na kutoa pasi za goli 4.

Mchezo wa jana dhidi ya Torino ulimalizika kwa Juventus kushinda 4-1 na kufikisha pointi 75 katika mechi 30 huku wakiongoza msimamo wa Ligi.