Jumapili , 29th Mei , 2016

Maelfu ya mashabiki na wapenzi wa soka nchini Hispania wamewapokea mabingwa wa kihistoria wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid ambao wamewasili hii leo wakitokea nchini Italia ambako walikwenda kucheza fainali ya kombe hilo dhidi ya Atletico.

Umati wa mashabiki wa timu ya soka ya Real Madrid wakiwalaki mashujaa wao.

Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya maarufu kama Uefa Champions League kwa mara ya 11, timu ya Real Madrid wamerejea kwao Hispania na kupokelewa kwa shangwe kubwa na maelfu ya mashabiki nchini huo ambao walijazana kila kona lilipopita basi lililowabeba mashujaa hao katika Jiji la Madrid.

Madrid wamerejea katika Jiji la Madrid saa chache baada ya kubeba ubingwa huo kwa mikwaju ya penati 5-3 dhidi ya wapinzani wao wakubwa wanaotoka mji mmoja Atletico Madrid katika mchezo mkali na mgumu mno uliochezwa kwa dakika 120.

Mechi ya fainali ilichezwa katika Jiji la Milan, kwenye Uwanja maarufu wa San Siro ilishuhudia timu hizo zikitoka sare ya goli 1-1 na kulazimika kufikia hatua ya mikwaju ya penati, fainali ambayo ilitazamwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani kote.