Jumanne , 22nd Feb , 2022

Klabu ya Real Madrid imeripotiwa kuungana na Manchester United katika harakati za kusaka saini ya kocha Mauricio Pochettino, ambaye anatarajiwa kuondoka Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu.

Kocha Mauricio Pochettino akielekeza jambo uwanjani dhidi ya Real Madrid.

Ikumbukwe Real Madrid pamoja na Tottenham, walishindwa jaribio la kumnasa Pochettino kutoka PSG msimu uliopita majira ya joto, kwasababu wababe hao wa Ligue one ya Ufaransa hawakuwa tayari kumruhusu Muargentina huyo kuondoka.

Lakini sasa kuna hisia inayotia moyo kwa Madrid kwamba Pochettino atapatikana mwishoni mwa msimu huu na wababe hao wa La Liga wametajwa kuweka tumaini lao kwa kocha huyo mkuu wa zamani wa Spurs huku mashaka yakiibuka kuhusu mustakabali wa Carlo Ancelotti Santiago Bernabeu.

(Carlo Ancelotti akielekeza jambo uwanjani kwenye mchezo dhidi ya PSG)

Wachezaji wa Los Blancos walikumbana na kejeli toka kwa mashabiki wao licha ya kupata ushindi wa magoli 3 kwa 1 dhidi ya Alaves Jumamosi iliyopita, huku kukiwa na taarifa kwamba Ancelotti anaweza kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu.

Matokeo watakayopata katika Ligi ya Mabingwa barani ulaya msimu huu, huenda yakawa na mchango mkubwa katika kufikia kufanya maamuzi kabla ya msimu ujao kuanza, huku rais Florentino Perez akitazamiwa kufufua nia yake ya kumnunua Pochettino iwapo Ancelotti ataondoka klabuni hapo.