Jumatatu , 18th Aug , 2014

Ziara yao itatoa funzo kwa vijana na itafungua fursa ya ushirikiano katika nyanja za kimichezo, kijamii na kiuchumi kwakuwa watatembelea pia baadhi ya vivutio vya utalii hapa nchini

Baadhi ya wachezaji wa timu ya magwiji wa Real Madrid watakaotua nchini kuanzia August 21 mwaka huu.

Kundi la kwanza la wachezaji nyota wa zamani kutoka kikosi cha Magwiji wa timu ya Real Madrid ya Hispania [Madrid Legends] linatarajia kutua nchini Alhamis ya juma hili tayari kwa maandalizi ya ziara ya siku Tano ya timu hiyo ya maveterani waliowahi kuwika na kufanya makubwa katika timu ya Real Madrid

Mratibu wa ziara hiyo Evarist Hagira amesema kikosi cha magwiji hao kitakamilika Ijumaa August 22 kwa kundi lililobaki kutua nchini ambapo Jumamosi watavaana na kikosi cha wachezaji magwiji wa Tanzania [Tanzania All Stars]
Hagira amesema kiujumla maandalizi yote ya ziara ya magwiji hao ambayo inajulikana kama utalii wa kimichezo hapa nchini yamekamilika

Hagira ametaja kundi la kwanza la baadhi ya wachezaji wanaotarajiwa kutua nchini katikati ya wiki hii ni pamoja na wakongwe Luis Figo, Michael Owen, Fabio Canavaro na Christian Kalembeu na kundi lingine ambalo litakuwa na wachezaji wengine na mashabiki wanaofikia 50 litatua August 22 siku ya Ijumaa ikiwa ni siku moja kabla ya timu hiyo kuvaana na timu ya nyota wa zamani waliowahi kuwika na vilabu mbalimbali vya hapa nchini kama kipa Mohamed Mwameja, beki Boniface Pawasa, Edibili Lunyamila na wengine wengi.