Alhamisi , 23rd Sep , 2021

Makocha wa vilabu vya Simba na Yanga wamezungumza kwa nyakati tofauti tofauti kuhusu maandalizi ya mchezo wa fainali ya Ngao ya Hisani ya Jamii unaotaraji kuchezwa Jumamosi ya Septemba 25, 2021 kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Kocha wa Simba, Mfaransa Didier Gomez (kushoto) na kocha wa Yanga, Mohammed Nasreddine Nabi (kulia).

Kocha wa Simba, Didier Gomez amesema hakuna mchezo rahisi katika haya mashindano na kila timu inafanya maandalizi kusaka ushindi hivyo wanapaswa kuwa makini ili wapate matokeo mazuri huku akiwa na imani ya kushinda kombe hilo na kuanza msimu vizuri.

"Nina Imani tutaanza msimu mzuri kwa kushinda taji, tumefanya maandalizi ya kutosha wakati huu. Tumejipanga kimbinu na tumeendelea kurekebisha makosa machache, pia tumeboresha maeneo tuliyokuwa bora ili kuhakikisha tunaanza msimu kwa kuchukua taji na kama  tulivyomaliza msimu kwa kushinda mataji"

"Hakuna mechi rahisi katika haya mashindano na kila timu inafanya maandalizi kusaka ushindi, tunapaswa kuwa makini ili tupate matokeo mazuri ambayo yatatupeleka katika hatua inayofuata"

Kwa upande wa kocha wa Yanga, Mohammed Nasreddine Nabi amesema wanahitaji kushinda mechi hiyo kuliko kitu kingine kwa sasa kwasababu hawakufanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika hivyo wameelekeza akili na mipango yote kwenye fainali hiyo na kukiri kuwa wapo tayari kuanza na rekodi nzuri katika msimu ujao.

"Tunahitaji kuahinda mechi hiyo kuliko kitu kingine kwa sasa, hatukufanya vizuri kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, sasa tumerejea kamili kwenye mashindano ya ndani, tunaanza na Ngao ya Jamii halafu akili na mipango itahamia kwenye ligi kuu Tanzania Bara"

"Tuko tayari, tunajua umuhimu wa kupata ushindi Jumamosi, tunataka kuanza na rekodi nzuri katika msimu wa mwaka 2021-22".

Mchezo huo utakuwa watatu kwa mapacha hao wa kariakoo kukutana kwenye kalenda ya mwaka 2021 baada ya kukutana Julai 3 kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi kuu na baadae Julai 25 kwenye fainali ya kombe la Shirikisho nchini huku Simba akiibuka bingwa kwa kupata ushindi wa bao 1-0 baada ya kufungwa 1-0 kwenye Ligi kuu.