Jumanne , 15th Feb , 2022

Kocha wa Simba SC Pablo Franco martin amesema malengo yao ni kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa kombe la Azam Sports Federation Cup kesho dhidi ya Ruvu Shooting, huku malengo ikiwa ni kutetea ubingwa wa michuano hii.

Kocha wa Simba Pablo Franco Martin

Simba ndio mabingwa watetezi wa michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa misimu miwili mfululizo na kesho Februari 15 watashuka dimbani kuminyana na Ruvu Shooting kwenye mchezo wa mtoano wa hatua ya 16 bora utakaochezwa uwanja wa Benjamini Mkapa Dar es salaam majira ya Saa 1:00 Usiku.

Kuelekea mchezo huo kocha Pablo amesema

“Sisi ndio mabingwa wa michuano hii na malengo yetu ni kuhakikisha tunavuka hatua hii na kwenda robo fainali na hatimaye tulitete kombe letu” Amesema Pablo

Kwa upande mwingine kocha huyo raia wa Hispania amezungumzia hali ya kikosi chake kuelekea mchezo wa kesho

“Kutakuwa na mabadiliko kidogo ya kikosi na tutaingia kivingine, baada ya mechi ya juzi hatujapata muda wa kuweka miili sawa (recovery) lakini tunahitaji kushinda. Tulikuwa katika kiwango bora kwenye mchezo uliopita. Tunakwenda kukutana na timu bora na hii ni mechi ya mtoano kwa hiyo tunapaswa kuhakikisha tunakuwa makini, ni muhimu kwetu kuingia hatua inayofuata,” amesema Pablo

Na inaripotiwa kuwa kikosi cha Simba baada ya mchezo wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting kitaondoka Dar es salaam kwenda nchini Niger kwa ajili ya mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya US Gendamerie utakaochezwa Februari 18, 2022.