Jumanne , 2nd Apr , 2019

Kwenye msimu huu wa 2018/19 wa EPL kama sio kuzidi basi utakuwa unalingana na msimu wa 2011/12 kwa maana ya ushindani unaoendelea kuoneshwa.

Man United na Spurs

Bingwa wa ligi katika msimu wa 2011/12 alikuwa ni Manchester City ambaye ilibidi kusubiri matokeo ya michezo ya mwisho kabisa ili kuweza kumpata mshindi, kwa wafuatiliaji wa ligi hii watakuwa wanakumbuka. Mazingira hayo yanaelekea kutokea katika msimu huu ambao hadi sasa kuna ushindani mkubwa wa aina tatu katika ligi.

Ushindani kwa kwanza upo katika mbio za ubingwa kati ya timu mbili, Manchester City na Liverpool ambazo kwa muda mrefu tangu mwanzoni mwa msimu zilitabiriwa ubingwa kutokana na aina ya vikosi vyao. Tofauti ya alama kati yao hivi sasa ni mbili lakini Man City ina faida zaidi ya kuipiku Liverpool kwa pointi moja kwakuwa bado ina kiporo.

Eneo la pili lenye ushindani ni la kumaliza 'Top Four' ambapo Arsenal, Tottenham Hotspurs, Chelsea na Manchester United zinawania nafasi nne za kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao. Arsenal imepanda hadi nafasi ya tatu baada ya ushindi wake dhidi ya Newcastle United, ikiishusha Spurs ambayo ilifungwa dhidi ya Liverpool, huku Manchester United ikiwa katika nafasi ya tano kwa kufungana pointi na Spurs na ikiwa na pointi moja mbele dhidi ya Chelsea iliyo katika nafasi ya sita.

Kwa haraka haraka kabla ya kuangalia eneo la mwisho la ushindani ambalo ni la kuporomoka daraja, tuangalie uwezekano wa Liverpool kuibuka bingwa kupitia Man United na Spurs.

Michezo iliyobaki kwa Liverpool na Man City

 

Manchester City imebakiza mechi 7 ambapo mechi mbili kati ya hizo ni dhidi ya Manchester United na Tottenham Hotspurs. Ushindani unakuja pale ambapo timu hizo zitakuwa zinapigania kupata nafasi ya kumaliza 'Top Four' huku Manchester City yenyewe ikiwa na kasi ya kufukuzia ubingwa.

Liverpool imebakiza michezo 6 kuelekea mwishoni mwa ligi, ambapo mechi moja kati ya hizo ni dhidi ya Chelsea ambayo nayo ipo katika vita ya kumaliza katika nafasi nne za juu. Vita hii inaelekea sehemu nzuri zaidi ambapo katika mbio za ubingwa, Liverpool ina faida zaidi kutokana na kuwa na mechi moja ngumu kuliko Man City ambayo ina mechi mbili ngumu kati ya zilizobakia. Je, Man United na Spurs zitakubali kupoteza dhidi ya Man City, au Chelsea itapoteza dhidi ya Liverpool kuhatarisha nafasi zao za kucheza Klabu Bingwa Ulaya?.

Sasa tumalizie na eneo la mwisho la ushindani katika ligi, ambalo ni la kuporomoka daraja. Kwenye eneo hili, jumla ya timu 6 zimo katika vita ya kuporomoka daraja, ambazo ni Huddersfield Town, Fulham, Cardiff City, Burnley, Southampton na Brighton. Huddersfield tayari imeshaporomoka daraja, ambapo hivi sasa bado timu mbili zitakazoungana na timu hiyo kwenda Championship.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.