Jumatatu , 30th Dec , 2019

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara hajauacha salama mchakato wa kumpata kocha mpya unaoendelea ndani ya klabu ya Yanga.

Haji Manara (kushoto), Hersi Said akiwa na kocha wa zamani wa Hispania Vicente del Bosque

Yanga inamsaka kocha mpya atakayerithi mikoba ya kocha Mwinyi Zahera ambaye aliachana na klabu hiyo mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2019, ambapo hivi sasa timu ipo chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa.

Manara ametupa vijembe kwa mahasimu wake kutokana na picha ambazo zinasambaa mtandaoni zikimuonesha Meneja Masoko wa GSM ambao ni wadhamini wa klabu hiyo akiwa na baadhi ya watu maarufu duniani wakiwemo makocha.

Picha hizo zinahusishwa na mchakato wa Yanga kumtafuta kocha mpya, mchakato huo ukifanywa na wadhamini hao ambao ndio watengenezaji wa jezi za Yanga lakini pia wakifanikisha sajili mbalimbali za dirisha dogo ndani ya klabu

Hayo yanajiri huku homa ya pambano la mahasimu wa jadi, Simba na Yanga ikizidi kupanda, zikiwa zimesalia siku tano kabla ya mchezo huo kupigwa katika Uwanja wa Taifa Jumamosi hii, Januari 4, 2020. Katika msimamo wa ligi, Simba inaongoza ikiwa na pointi 31 baada ya kushuka dimbani michezo 12 huku Yanga ikiwa katika nafasi ya tano baada ya kukusanya pointi 21 katika michezo 10.