Ijumaa , 16th Nov , 2018

Baada ya kusambaa kwa tetesi za kiungo wa klabu ya Simba, Haruna Niyonzima kutakiwa na klabu ya Azam Fc, hatimaye Afisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara ameibuka na kuzikanusha.

Haji Manara (kushoto), Haruna Niyonzima (kulia)

Kupitia katika ukurasa wake wa Instagram, Haji Manara amesema kuwa hawana mpango wa kumuacha mchezaji huyo kwakuwa yupo katika mipango yao.

"Haruna Niyonzima yupo 'camp now' na leo atacheza ikimpendeza kocha dhidi ya Nyasa Big Bullets," amesema.

Kikosi cha Simba kinashuka dimbani leo kuvaana na Nyasa Big Bullets ya nchini Malawi katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, ikiwa ni katika maandalizi ya michuano ya klabu barani Afrika 2018/19 inayotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Katika michuano hiyo, Simba itavaana na Mbabane Swallows ya Swartzland, kati ya Novemba 27 na 28 huku wapinzani wao wa leo, Nyasa Big Bullets ikicheza na Gor Mahia ya Kenya.