Jumatatu , 29th Nov , 2021

Mchezo kati ya Chelsea na Manchester United ulimalizika usiku wa jana kwa sare 1-1 kwenye dimba la Stamford Bridger huku wenyeji Chelsea wakilazimika kusawazisha ili kukwepa kipigo kingine kwenye EPL.

(Jado Sancho akimtoka Jorginho na kwenda kufunga bao la Man United)

Manchester United ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa winga wake Jadon Sancho dakika 50 kufuatia Jorginho kuboronga kabla ya Jorginho kurekebisha makosa yake kwa kufunga bao kwa mkwaju wa penalty dakika 69.

Sare hiyo imeifanya Chelsea kuzidi kuwa na rekodi mbovu mbele ya Manchester United kwenye EPL pekee kwani mchezo huo umefanya Chelsea kushindwa kupata ushindi kwenye michezo nane ya mwisho ya EPL dhidi ya Man United.

Wawili hao wametoa sare tano na Chelsea ikipoteza michezo mitatu. Mara baada ya mchezo huo kumalizika kocha wa muda wa Manchester United, Michael Carrick amesema Chelsea haikustahili kupata penalty huku Tuchel akichekelea.

Carrick amesema, "Sijafurahishwa kusema ukweli. Kama ukiwa unaongoza wa bao moja kwenye mchezo kama huu, alafu ukapoteza uwezekano wa kupata ushindi, Inavunja moyo. Najivunia wachezaji hawa kwa juma hili nililokuwa nao”.

“Tulijaribu kufanya kitu kizuri kwenye wakati mgumu, lakini ndiyo hivo tumepata hisia tofauti. Tulikuja kwa ajili ya kushinda mchezo. Tumevunjika moyo kidogo, Siwezi kusema uongo" Alimalizia hivyo Carrick.

Kwa upande wa kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amesema, "Wajilinda sana na huenda tulipaswa kupata bao la mapema ili kuifungua safu yao ya ulinzi.”

“Walipata kujiamini na uhuru kwa asilimia kubwa kufuatiwa na nafasi nyingi kwenye goli letu. Lakini kiujumla, ninafuraha sana kwa namna tulivyocheza. Nilivutiwa nanamna tulivyoutaka mchezo, kiwango chetu cha ari na kasi"

Kwa sare hiyo Chelsea imesalia kinara wa EPL akiwa na alama 30 alama moja mbele ya Manchester City wakati Manchester United wakiwa nafasi ya nane na alama zao 18.