Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Mlinda mlango namba moja wa timu ya Simba Aishi Salum Manula, amesema kuwa wanajipanga vyema kuelekea mchezo wao wa hatua ya kwanza ya michuano ya kombe la shirikisho barani Africa dhidi ya Al Masry ya Misri.

Akiongea katika mahojiano na mtandao wa klabu hiyo Manula amesema baada ya kuitoa Gendarmerie ya Djibouti sasa ndio mashindano yameanza rasmi hivyo ni lazima wajiandae kikamilifu ili timu hiyo ifanye vizuri.

''Michezo yetu miwili dhidi ya Gendarmerie Ilikuwa ni michezo ya kawaida sana ila nadhani sasa kwenye mchezo unaofuata ndio tunaanza mashindano rasmi na tunajiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Al Masry ambapo tutaanza nyumbani hivyo lazima tushinde'', amesema.

Aidha Manula amesema kikosi cha Simba hivi sasa kipo kwenye ubora na kina benchi la ufundi ambalo ni bora hivyo anaamini kitafanya vizuri kwenye mchezo huo wa Machi 6 uwanja wa taifa Dar es salaam kabla ya kusafiri kwenda Misri Machi 6.

Simba kwasasa inaendelea na maandalizi ya mchezo wake wa jumatatu, ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mbao FC utakaopigwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.