Ijumaa , 25th Jan , 2019

''Watu hawajui kama wewe ni shabiki yangu kabla hajakuja Steven nadhani zile vurugu zinaendana sasa na wimbo si eti?''.

Barnaba Classic

Ni ujumbe wa Barnaba baada ya mzazi mwenzake (Zuunamela), kujirekodi video akicheza wimbo wake mpya unaoitwa Washa, ambapo mashairi yake wengi wanayatafsiri kama yanamlenga mama mtoto wake huyo.

Tangu wawili hao waaachane nyimbo kadhaa za Barnaba ambazo ameachia zimekuwa na ujumbe unaohusu watu wapenzi kuachana huku mmoja akionesha kuwa atazoea na wala haumizwi na kuachana huko.

Kwa mfano katika wimbo wa 'mapenzi jeneza' uliotoka Septemba 19, 2017 kuna mstari Barnaba anaimba, ''sina budi kukubaliana na uamuzi aliochukua, kama mpenzi nitapata mwingine na nafsi itatulia''.

Wakati kwenye ngoma ya 'Tuachane mdogo mdogo', ukiacha jina la wimbo kuna mistari kama, ''nahisi nimeonewa kwa haya niliyofanyiwa, penzi langu bembea wamebembea wengine''.

Ngoma yake aliyotoa wiki hii ya Washa nayo imekuwa gumzo kutokana na aina ya mashairi aliyoimba humo mfano, ''ukiachwa achika, ukimwagwa mwagika na ukitemwa temeka, penzi bovu yanini kung'ang'ania ?''.

Yote kwa yote Barnaba anafanya kazi ya sanaa ambayo inaangazia masuala mbalimbali kwenye jamii hivyo sio lazima alichokiimba kiwe kinahusu maisha yake. Unaweza kuwa ni ubunifu tu ukizingatia yeye ni moja ya waandishi bora wa mashairi katika muziki wa Bongofleva.