Jumatatu , 17th Jan , 2022

Mshambuliaji wa Manchester United, Anthony Martial, amekanusha madai ya Kocha Mkuu Ralf Rangnick kwamba hakutaka kuwa sehemu ya kikosi kilichotoka sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Aston Villa.

Martial ambaye amepoteza nafasi yake kwenye kikosi cha United baada ya ujio wa Cavani na Ronaldo, anataka kuondoka ndani ya Manchester United na timu unayotajwa kuisaka saini yake ni Sevilla ambayo inahitaji kupata huduma yake.

Katika Uwanja wa Villa Park, United ilikuwa na wachezaji nane benchi kisha baadaye Rangnick akizungumza na waandishi wa habari za michezo, Kocha huyo raia wa Ujerumani aliweka wazi kuwa Martial hakutaka kuwa sehemu ya kikosi.

“Hakutaka kuwa sehemu ya kikosi, kwa kawaida angekuwepo lakini hakutaka hiyo ni sababu ambayo hakusafiri nasi''. alisema Rangnick

Baada ya kuibuka kwa taarifa hiyo Martial raia wa Ufaransa kupitia katika mitandao aliandika: "Kamwe sitaweza kukataa kuichezea Man United. Nimekuwa hapa kwa miaka 7 na sijawahi na sitawahi kutoiheshimu klabu na mashabiki,". alisema Martial.