Ijumaa , 6th Mei , 2016

Mwenyekiti wa Timu ya Mbeya City FC Mussa Mapunda amelipongeza Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa hatua yake ya kuipoka pointi 3 timu ya Azam FC na kuziweka kwa timu yake kufuatia makosa yaliyofanywa na timu hiyo.

Mapunda amesema, kwa kosa hilo Mbeya City ilistahili kupata ushindi huo wa bao 3 na pointi 3 kama TFF walivyotenda haki kwa kufuata kanuni za ligi zinavyoelekeza na kutoa angalizo kwa vilabu vyote vinavyoshiriki Ligi Kuu Tanzania bara kuongeza umakini katika kutunza kumbukumbu za adhabu au makosa mbalimbali kwa wachezaji wake.

Kwa upande mwingine Mapunda amesema, bado anaamini TFF itaitendea haki Mbeya City kwa kuchukua hatua kama hizi kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union uliovunjika dakika za mwisho za kipindi cha pili baada ya kutokea kwa vurugu kubwa uwanjani zilizosababishwa na mashabiki wa timu hiyo ya Mjini Tanga.