Ijumaa , 28th Aug , 2020

Mshambuliaji wa Klabu ya Simba, Meddie Kagere amesema kiu ya kufanikiwa kila siku ndiyo inamfanya aendelee kujinoa maradufu ili aendelee kutwaa tuzo ambazo ni heshima kubwa kwa mchezaji.

Mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Meddie Kagere akionyesha ishara ya kukubaliana na jambo katika mchezo wa VPL.

Kagere ambaye aliibuka mfungaji bora msimu uliomalizika akiwa amepachika mabao 22 katika VPL, amesema nia yake ni kubeba tuzo zinazotolewa na taasisi mbali mbali ambazo pia zinaambatana na kiasi cha fedha, na anaamini vitu hivyo humjenga mchezaji yoyote na siku zote fedha huwa hazitoshi.

Kuhusu yeye kufunga mabao Kagere amesema''Siwezi kusema mimi ni bora sana,nadhani goli linapatikana iwapo mmoja anafanya makosa,hata mimi huwa nakosa bao tena la wazi,hivyo hata mabeki huwa wanajiandaa lakini makosa ni sehemu ya mchezo,halafu pia hata wao wakinisoma kwa vile wananiona,hivyo mimi huwa nabadilika kila mara ili wasijue namna ya kunidhibiti''

Alipoulizwa kuhusu nafasi yake kikosini wakati msimu unakaribia kumalizika Kagere amesema''Kila kitu ni mpango wa Mungu ,huwezi jua kipi kitatokea katika maisha yako mbele,inawezekana mimi ningepanga kufunga mabao mengi iwapo ningepata nafasi ya kucheza,lakini huenda mambo yangekua tofauti,labda ningeumia,au kocha angenipumzisha,hivyo lolote linaweza kutokea''

Vilevile Kagere anazungumziaje kuhusu ongezeko la wachezaji katika idara yake ?''Kila mtu atafanya mazoezi,na hakuna mchezaji ambaye kwa sasa ana uhakika wa namba,tukishaanza mazoezi kocha ataamua ni yupi ataanza,na hata kama atampanga mchezaji mwingine,binafsi sioni tatizo kwa kuwa cha muhimu ni mafanikio ya Timu kuliko mchezaji,Timu kwanza''

Katika hatua nyingine Kagere alisita kuzungumzia ujio wa mshambuliaji mwenzake pacha wa zamani katika Klabu ya Gor Mahia ya Kenya, Jaqcuise Tuyisenge ambaye anahusishwa na kuja nchini Tanzania huku Yanga na Sima zikihusishwa na usajili wake.

TAKWIMU ZAKE

Kagere alifunga mabao 45 katika misimu miwili katika ligi kuu ya soka Tanzania bara .