Jumanne , 8th Dec , 2020

Mahasimu wawili wa muda mrefu Mshambuliaji nyota wa klabu ya Barcelona Lionel Messi na Crsitiano Ronaldo nyota wa klabu ya Juventus wanatarajia kuunogesha usiku wa michuano ya mabingwa barani ulaya wakati vilabu vyao vikitazamiwa kukutana usiku hii leo.

Mchezo wa usiku wa leo utakuwa ni wa 36 Lionel Messi na Crsitiano Ronaldo wanakutana kwenye ngavi zote klabu na timu ya taifa

Barcelona ambaye ni kinara wa kundi G akiwa na alama 15 baada ya kushinda michezo yote mitano ya hatua hiyo ya makundi atakuwa mwenyeji wa klabu ya Juventus ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 12 mchezo unaotaraji kupigwa katika dimba la Camp Nou mishale ya saa 5 kamili usiku.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha wa Barcelona, Reonald Koeman, amethibitisha uwepo wa Messi ambaye alimpumzisha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Dynamo Kiev, Keoman amesisiiza wanahitaji ushindi ili waendelee kuwa vinara wa kundi hilo huku akikiri wanayo kazi kubwa ya kufanya hivyo.

Kwa Upande wa kocha wa Juventus Andrea Pirlo, amesema mchezo huo ni mgumu sana kwao na kazi kubwa waliyonayo ni kujitahidi kujilinda kama timu ili kuweza kuibuka na alama tatu ugenini. Barcelona na Juventus wote wameshafuzu kutinga hatua inayofuata ya 16 bora.

Hii inatakuwa ni mara ya 36 Messi na CR7 kukutana kwani tayari wameshakutana mara 2 kwenye michezo ya kirafiki ya timu zao za taifa mwaka 2011 ambapo Argentina alipata ushindi wa 2-1 wawili hao wote wakafunga bao kwenye mchezo huo na mwaka 2014 ambapo Ureno ilishinda bao 1-0.

Kwenye ngazi ya vilabu Messi na CR7 wameshakutana mara 33, mara 3 CR7 akiwa na klabu ya Man Utd na mara 30 wakikutana kwenye El Classico nchini Uhispania baada ya CR7 kuhamia Real Madrid mwaka 2009 na kuondoka mwaka 2018.

Tokea wawili hao wakutane mara 35 ni Messi ambaye ameondoka na ushindi mara nyingi kuliko CR7 kwenye michezo yao, Messi amepata ushindi mara 16, CR7 mara 10 na kutoka sare mara 9.

Vilabu vilivyofuzu na kuungana na Barcelona na Juventus ni pamoja na Chelsea, Sevilla, Borussia Dortmund, Bayern Munich, Liverpool, Manchester City na FC Porto.