Jumanne , 27th Oct , 2020

Kocha wa Klabu ya Ruvu Shooting ya Pwani, Charles Boniface Mkwasa amesisitiza kwamba vilabu vinatakiwa kuwapa nafasi wachezaji wazawa kwakuwa wanauwezo mkubwa wa kucheza mpira wa miguu.

Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa akiwa kibaruani

Kauli ya Mkwasa' Master ' inakuja muda mchache baada ya kikosi chake kuiadhibu Simba ambayo imekusanya wachezaji wengi wa kigeni lakini walishindwa kufua dafu mbele ya Ruvu Shooting ambayo haikua na mchezaji wakigeni hata mmoja.

''Niseme ukweli haikuwa mechi rahisi, lakini kama ilivyo kawaida, mara nyingi mkubwa huwa hawezi kumfuatilia au kumsikiliza mdogo lakini mdogo marazote anamsikiliza mkubwa hata kama anakosea.

Sisi tuliwasoma Simba vyema, na tukang'amua udhaifu wao licha ya ubora wao na tukawafunga kama mnavyoona''.Mkwasa.

Katika hatua nyingine kocha huyo wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' alifunguka na kusema kwamba vilabu vikongwe haviwaamini wachezaji wazawa.

''Nasisitiza kwamba timu zenu ziwape nafasi wachezaji wazawa, mnang'ang'ania wageni, mnawanyima nafasi watanzania, kwenye vilabu vyenu wanacheza dakika tano halafu mnatarajia waipe matokeo mazuri timu ya taifa haiwezekani. Mimi si mmeona vijana wangu wazalendo walichokifanya, wanaweza sana'' Alimalizia Mkwasa.

>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>