Jumatano , 22nd Mar , 2017

Katibu Mkuu wa timu ya Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa amesema timu yake imejipanga vyema kuelekea mchezo wao dhidi ya MC Alger kutoka Algeria na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kutokuwa na hofu.

Boniface Mkwasa

Mkwasa amesema licha ya wapinzani wao kuwa na historia nzuri, hawezi kuogopa hilo na amedhamiria kuifunga hapa nyumbani ili watakapoenda kwao wasiwe na kibarua kigumu.

“Mechi kama hizi unapopata ushindi mzuri wa nyumbani, basi unapunguza mlima wa kuupanda ugenini. MC Alger ni timu nzuri na amekuwa bingwa wa Afrika hivyo kila mtu atataka kuiona, na sisi tunawaheshimu kwa historia yao lakini tunakwenda kupambana kutafuta ushindi." Alisema Mkwasa

Aidha Mkwasa amesema mpaka sasa hajafahamu mechi hiyo itachezewa wapi ila muda utakapofika watu wataambiwa ni wapi ila wao popote watakapopangiwa wapo tayari kucheza.

"Muda ukifika tutawajuza wapi mechi itafanyikia kama ni hapa jijini au popote Tanzania. Kwa sasa bado hatujaamua lolote katika hilo hivyo uwanja wa taifa unabaki kutambulika kama uwanja wa nyumbani". Alisisitiza Katibu huyo

Kwa upande mwingine amewataka mashabiki na wadau wote wa soka nchini kuipa sapoti timu hiyo muda wote wa dakika 90 za mchezo bila ya kuogopa mbwembwe za wapinzano wao wanapokuwa wameuteka mpira miguuni mwao.