Jumapili , 10th Dec , 2017

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho ataiongoza timu yake kukabiliana na vinara wa ligi hiyo mahasibu wao Manchester City huku akiwa na kazi ya kulipa kisasi na kupunguza rekodi ya kufungwa na kocha Pep Guardiola.

Mchezo huo wa ligi kuu soka ya EPL utapigwa katika dimba la Old Trafford leo majira ya saa moja jioni ambapo Manchester United ina rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja katika mechi 40 mfululizo katika uwanja huo.

Hata hivyo pamoja na kuwa na rekodi hiyo lakini timu ya mwisho kuifunga Manchester United katika uwanja wake wa nyumbani ilikuwa ni Man City na ilikuwa msimu uliopita katika mchezo uliopigwa Septemba 2016.

Manchester City haijapoteza mchezo msimu huu ambapo tayari wana rekodi ya kushinda mechi 13 mfululizo, na endapo watashinda mchezo wa leo wataifikia rekodi ya Arsenal (The Invicibles) ya kushinda mechi 14 mfululizo za ligi msimu wa 2003.

Tangu waanze kukutana makocha hao wawili wanaosifika kwa mbinu, wamecheza mechi 19, ambapo Guardiola ameshinda mechi 9, wakati Mourinho ameshinda mechi 4 na wametoka sare mechi 6. Je leo Guardiola ataongeza rekodi au Mourinho atapunguza?.