Jumatano , 25th Mei , 2022

Mshambuliaji wa zamani wa vilabu vya Simba na Yanga, Amisi Tambwe amesema wakati mwingine maoni yanayotolewa na wadau wa mpira nchini kuhusu maendeleo ya mchezo wenyewe huwa yana athiriwa na msukumo wa upande wa mtu anaoushabikia au anaoutumikia katika wakati husika.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Amisi Tambwe alipokuwa anakabidhiwa mpira kwa kufunga Hat-Trick

Akizungumza na kipindi cha michezo cha Kipenga cha East Africa Radio kinachoruka kila siku za wiki kuanzia saa 2-3 usiku, Tamwe amesema mpira wa Tanzania umetawaliwa na mapenzi ya Simba na Yanga kuanzia kwa Viongozi, Waamuzi, Wachezaji na hata Waandishi wa Habari.

Kauli hiyo ameitoa alipoulizwa juu ya maoni yaliyotolewa na baadhi ya wadau kuhusu udhaifu wa Ligi yetu ambapo Tambwe amesema si kweli kwamba Ligi ya Tanzania ni dhaifu bali aliyetoa mtazamo huo alitawaliwa na mapenzi ya timu anayoiongoza au ishabikia.

''Ligi ni ngumu sana na si dhaifu, tena ipo juu, lakini kama unavyojua mpira wa Tanzania ni Siasa, ni Simba na Yanga, hata Viongozi ni Simba na Yanga, Waamuzi ni Simba na Yanga, hata Wachezaji ni Simba na Yanga''alisema Tambwe.

Katika hatua nyingine nyota huyo wa kimataifa wa Burundi ambaye amekuwa na mchango mkubwa ulioisaidia DTB kupanda Ligi Kuu, amesema wamejipanga kufanya makubwa katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara.