Jumamosi , 2nd Jun , 2018

Klabu ya Mtibwa Sugar yenye makao makuu yake Turiani Manungu Morogoro, imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho nchini (ASFC), na kuwanyima Singida United rekodi ya kupanda ligi na kushinda taji.

Mabao 3-2 kwenye mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa yametosha kuifanya Singida United ifanane na Mbao FC ya Mwanza ambapo nayo ilipanda daraja msimu wa kwanza na kufika fainali ya ASFC lakini ikafungwa na Simba.

Mtibwa sasa imekuwa timu ya tatu kutwaa ubingwa huo tangu urejeshwe rasmi msimu wa 2015/16 ambapo Yanga ilitwaa huku Simba wakitwaa msimu wa 2016/17 na sasa Mtibwa msimu wa 2017/18.

Hata hivyo bado kuna sintofahamu juu ya mabingwa hao wapya wa Kombe la Shirikisho nchini juu ya uwakilishi wao katika michuano ya kimataifa kutokana na kuwepo kwa adhabu ya kufungiwa na CAF huku wao wakidai kuwa adhabu hiyo ilishafutwa.

Kwa upande mwingine Singida United wameshindwa kuwapa rekodi wachezaji wao Manyika Jr, Deus Kaseke na kocha Hans Van Pluijm ya kutwaa ubingwa kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo wakiwa na timu zao za zamani.