Mwakalebela azungumzia nafasi ya Dismas Ten Yanga

Jumatano , 14th Aug , 2019

Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrik Mwakalebela amemaliza utata juu ya tetesi za uongozi wa klabu hiyo kutokuwa na maelewano mazuri na Kaimu Katibu Mkuu wake, Dismas Ten.

Fredrick Mwakalebela (katikati), Dismas Ten (kushoto) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Araphat.

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari, amakao makuu ya klabu hiyo jana, Mwakalebela amesema kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya uongozi na Dismas na kwamba yeye kwa sasa anafanya kazi ya Ukaimu Katibu Mkuu na siyo ya usemaji/Afisa Habari.

"Dismas Ten ni Kaimu Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga kwahiyo kuna majukumu anayafanya kwa mujibu wa maagizo na kwa hivi sasa yeye si msemaji tena wa Yanga. Anachokifanya ni kutekeleza maagizo kutoka kwa Mwenyekiti kupitia kwa Makamu Mwenyekiti hadi kwake", amesema.

"Sekretarieti mpya inakuja na kama mnavyofahamu tumeshatangaza nafasi za kazi na mchakato unakwenda vizuri, tukishapa mtaiona safu nzima ya uongozi", ameongeza.

Aidha Mwakalebela ameitaja idara mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo ambazo zitajazwa watu hivi karibuni. Miongoni mwa nafasi hizo ni pamoja na Katibu Mkuu wa klabu, Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama, Mkurugenzi wa Mashindano, Mkurugenzi wa Ufundi, Idara ya Fedha na Utawala pamoja na Idara ya Masoko na Mauzo ambayo ndani yake itakuwa na kitengo cha Habari na Mawasiliano.