Mwigulu afichua Singida United kuifaidisha Yanga

Jumatano , 7th Aug , 2019

Mbunge wa Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Nchemba amefichua siri ya namna usajili wa klabu ya Singida United na unavyofaidisha klabu ya Yanga.

Dkt. Mwigulu Nchemba

Mwigulu ameelezea jinsi alivyofanikisha usajili wa wachezaji kadhaa na kuwapeleka Yanga, huku akisisitiza kuwa tangu klabu ilipokuwa daraja la kwanza amekuwa akifanya usajili mwenyewe, hivyo halina madhara yoyote kwake.

"Kila la heri wananchi, nilimsajili Fei Toto na kumtoa, na mwaka huu nimemsajili Ally Mtoni nikawapa Yanga na niliridhia Marcello asajiliwe Yanga. Watu wanaona kama ina madhara Singida United kufanya hivyo. Ukweli ni kwamba miaka yote tangu daraja la kwanza, Singida nasajili mwenyewe wachezaji wote na benchi la ufundi kwa gharama zangu", amesema Dkt Mwigulu.

"Naendesha klabu mwenyewe na mwaka huu Singida nimesajili kikosi bora kuliko cha mwaka jana, kikwetu kijana ukishakua na mji wako, wakati wa kilimo lazima utenge siku moja kwenda kulima shambani kwa baba yako. Ni suala la adabu tu na kufanya hivyo si kutelekeza famila yako", ameongeza.

Yanga ipo kambini Zanzibar kujiandaa na mchezo wa hatua ya kwanza wa Klabu Bingwa Afrika wikiendi hii dhidi ya Township Rollers katika uwanja wa taifa.