Jumatano , 20th Jan , 2021

Kundi la timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kundi D, kwenye michuano ya CHAN, limeweka rekodi ya kuwa na mabao mengi kuliko makundi yote tangu kuanza kwa michuano hiyo, inayoendela nchini Cameroon, kundi hilo limezalisha jumla ya mabao 5 kwenye michezo 2.

kiungo wa timu ya Taifa ya Zambia Collins Sikombe akiifungia zambia bao la kwanza kwa mkwaju wa penati kwenye ushindi wa bao 2-0 dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania Taifa stars

Taifa Stars ndio ilikuwa timu ya kwanza kuruhusu mabao mawili kwenye fainali za CHAN kwa kufungwa na Zambia mabao 2-0, kwenye mchezo wa kundi D, na tukashuhudia ushindi mkubwa wa kwanza kwenye michuano hiyo, kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo ambapo Guinea waliifunga Namibia mabao 3-0.

Sasa kundi hilo ndilo lililozalisha mabao mengi zaidi kuliko makundi yote kwenye fainali hizo likiwa limezalisha mabao 5, wakati kundi linalofuata kuwa na mabao mengi ni kundi A, ambalo limezalisha mabao 2, katika michezo yake 2 ya awali ambapo wenyeji Cameroon walishinda bao 1-0 dhidi ya Zimbabwe, na Mali wakaifunga Burkina Faso 1-0.

Kundi B na C yote yamezalisha bao moja moja, kwenye kundi B michezo yake ya kwanza ilizalisha bao 1 tu ambapo DR Congo waliifunga Congo Brazavill 1-0, na mchezo mwingine wa kundi hilo kati ya Libya na Niger ulimalizika kwa suluhu. Bao la pekee kwa kundi C lilifunga na timu ya taifa ya Morocco kwenye ushindi walioupata wa 1-0 dhidi ya Togo, na Rwanda na Uganda wakatoshana nguvu kwa mchezo wao kumalizika kwa suluhu.

Mpaka sasa yamefungwa jumla ya mabao 9 kwenye mashindano haya huku mabao 5 yakiwa yametoka kwenye kundi D, na kwa ujumla mashindano haya yana wastani wa bao 1.13 kufungwa kwa kila mchezo kwenye michezo 8 iliyochezwa mpaka sasa.

Fainali hizo zitaendelea tena leo kwa michezo miwili ya kundi A, wenyeji Cameroon watacheza dhidi ya Mali mchezo utakaochezwa Saa 1:00 Usiku na Burkina Faso wataminyana na Zimbabwe Saa 4:00 Usiku.