Alhamisi , 23rd Jul , 2020

Chama cha Mchezo wa Netball Tanzania CHANETA kimesema kuanzia mwaka ujao kitaandaa mechi nyingi za kirafiki na mashindano ya kimataifa ili kutafuta viwango vya juu vya ubora wa mchezo huo.

Kikosi cha timu ya taifa ya Netball ' Taifa Queens'

Chama cha mchezo wa Netball Tanzania CHANETA kimesema kuanzia mwaka ujao kitaandaa mechi nyingi za kirafiki na mashindano ya kimataifa ili kutafuta viwango vya juu vya ubora wa mchezo huo.

Akizungumza na EA TV Mwenyekiti wa CHANETA Dkt Devotha Marwa amesema kwa kipindi kirefu Tanzania imeshindwa kushiriki mashindano ya netball kimataifa kufuatia kufungiwa, kabla ya mwaka uliopita kushindwa kushiriki michuano ya Afrika kutokana na ukata, lakini wanajipanga upya kwa mwakani kucheza mechi nyingi za kirafiki na mataifa yenye viwango vya juu ili kupata alama zitakazoiinua Tanzania viwango vya juu.

''Tutaomba michezo ya kirafiki na timu zenye viwango vya juu kama Malawi, ili tukiwafunga tunapata alama za juu, hivyo kiwango chetu kinaongezeka kidunia." Alisema Marwa.

Mara ya mwisho Tanzania ilikuwa ya 15 kidunia kwenye viwango vya netball kabla ya kuporomoka na kutokuwepo kabisa kwenye viwango vya sasa.

Afrika kwa sasa kwenye viwango vya Dunia vya netball inabebwa na timu za Afrika Kusini (5), Malawi (6) na Uganda (7).