Jumatano , 3rd Feb , 2021

Taarifa kutoka chanzo cha kuaminika nchini Brazil, zinaripoti kuwa mshambuliaji wa klabu ya PSG ya Ufaransa na timu ya Taifa ya Brazil, Neymar Jr amefikia makubaliano ya kusaini kandarasi mpya ya miaka minne kuendelea kusalia PSG hadi mwaka 2026 na taarifa hizo kuwekwa wazi hivi karibuni.

Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi (kushoto) na Mshambuliaji wa PSG, Neymar Jr (kulia).

Taarifa hiyo imedukuliwa na Marcelo Bechler na kuipeleka kituo cha televisheni cha TNT Sports nchini Brazil ambacho kimesambaza taarifa hizo.Ikumbukwe kuwa, Bechler ndiye aliyekuwa mwandishi wa kwanza kutoa taarifa za Neymar kuihama Barcelona na kutimkia PSG mwaka 2017.

Suala la Neymar kusalia PSG zilipewa nguvu na Neymar mwenye baada ya kukiri kuwa na furaha klabuni hapo katikati mwa mwezi Januari mwaka huu. “Nina furaha sana PSG kwasasa. Mambo mengi yamebadilika sana, Ninataka kuendelea kusalia msimu ujao na nina imani Kylian Mbappe atasalia”.

Neymar kusalia na miamba hiyo ya soka nchini Ufaransa huenda ikawa rahisi kwa nyota huyo kumshawishi Lionel Messi kuhamia kwenye kikosi hiko baada ya kukiri ndoto yake kubwa ni kucheza na mkali huyo wa Catalunya baada ya kucheza naye kwa mafanikio makubwa sana.