Alhamisi , 28th Mei , 2015

Timu ya Taifa ya ngumi za Ridhaa ya Tanzania iliyotakiwa kuondoka hapo jana kuelekea nchini Zambia imekwama kuondoka kutokana na kushindwa kukamilisha baadhi ya vitu kwa ajili ya safari hiyo.

Katika taarifa yake, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi la Tanzania BFT, Wililo Lukelo amesema, mpaka jana shirikisho hilo lilikuwa bado halijapata kiasi chote cha fedha ili kufanikisha safari hiyo.

Lukelo amesema, mabondia hao walitakiwa kuondoka hapo jana kwa ajili ya kuelekea nchini Zambia kushiriki mashindano ambayo ni ya mwaliko yatakayofanyika Mei 30 mwaka huu kwa kushirikisha timu za Taifa kutoka nchi za Namibia, Angola, Botswana na wenyeji Zambia.

Lukelo amesema, wadau mbalimbali wanatakiwa kujitokeza kusaidia timu hiyo ili iweze kufanikiwa kushiriki mashindano hayo kwani itakuwa fursa nzuri ya kujipima kabla ya kushiriki mashindano ya All African Games yatakayofanyika Septemba mwaka huu nchini Congo Brazzaville.