Jumatano , 8th Apr , 2020

Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa kutokana na uzoefu wa kazi alio nao, anaweza kufanya kazi katika Shirikisho la Soka Duniani FIFA kama msemaji.

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara

Amesema hayo katika mahojiano na kipindi cha Kipenga Xtra cha East Africa Radio leo Aprili 8, na kusisitiza kuwa hakukuwa na haja ya kufanyiwa usaili wa kazi ya Afisa Habari wa Klabu ya Simba kutokana na uzoefu wake kutokuwa na shaka.

"Mimi uzoefu wangu wa kazi unajulikana, hata kazi ya kuwa Afisa Habari pale Simba sikufanyiwa 'Interview' kwa sababu hawakuwa na shaka na mimi, nani kwanza anayeweza kunifanyia mahojiano", amesema Manara.

"Kwenye suala la uwezo wa kazi pamoja na vyeti, mimi nina uwezo wa kuwa msemaji wa taasisi yoyote hapa Tanzania na kwenye mpira ninaweza kuwa hata msemaji wa FIFA", ameongeza.

Pia Haji Manara amezungumzia kuhusu suala la pesa za uwekezaji ndani ya klabu ya Simba, kama inavyozungumzwa na baadhi ya watu, ambapo amesema wenye haki ya kuhoji ni wanachana na mashabiki.

"Wenye uhalali wa kuhoji kuhusu Bilioni 20 za mwekezaji wa Simba ni mashabiki wenyewe ambao walimpa timu, siyo mtu mwingine tu ambaye hana uhalali", amesema.