Ninja afanya kama Yanga huko LA Galaxy

Jumatatu , 19th Aug , 2019

Beki mpya wa klabu ya LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Marekani MLS, Abdallah Shaibu 'Ninja' amecheza mchezo wake wa kwanza akiwa na timu hiyo hapo jana na kufanya makosa kama alivyofanya katika mchezo wa kwanza akiwa na Yanga.

Abdallah Shaibu Ninja

Awali, Ninja alisaini miaka minne na klabu ya Ligi Daraja la Tatu ya Jamhuri ya Czech na kisha kupelekwa kwa mkopo katika klabu ya LA Galaxy ya nchini Marekani ambako atacheza kwa msimu mzima.

Katika mchezo wake wa kwanza kati ya LA Galaxy na New Mexico, ambao umemalizika kwa sare ya 2-2, Abdallah Shaibu 'Ninja' alisababisha penalti katika dakika ya 76 ya mchezo baada ya kumchezea rafu mchezaji wa New Mexico.

Kwenye mchezo wake wa kwanza na klabu yake ya zamani ya Yanga, pia Ninja alisababisha bao kwa wapinzani wao Ruvu Shooting baada ya kujifunga kwenye mchezo wa kirafiki ulipigwa Agosti 12, 2017.

Lakini mchezaji huyo ameonekana kuaminiwa mapema na klabu yake mpya ya LA Galaxy kiasi cha kuchezeshwa katika kikosi cha timu ya pili ya klabu hiyo (LA Galaxy II), jambo linaloweza kumpa mwanga zaidi wa kujifunza na kurekebisha makosa madogo madogo ili kufanya vizuri na hata kucheza kikosi cha kwanza.